Rais wa shirikisho la vyama vya soka barani
Ulaya-Uefa, Michel Platini amesema kuwa
fainali za kombe la dunia za mwaka 2022
nchini Qatar lazima zichezwe kipindi cha
majira ya baridi.
Mchezaji huyo wa zamani wa Ufaransa
amejiweka katika upinzani dhidi ya baadhi ya
vilabu vikubwa vya soka barani Ulaya
ambavyo vimesisitiza kuwa fainali hizo
zipangwe mwezi May 2022.
Kwa kawaida fainali za Fifa za kombe la
dunia huwa zinachezwa kati ya mwezi Juni na
Julai, lakini Fifa imeambiwa kuwa katika
majira hayo nchini Qatar kunakuwa na joto
kali litakalowaweka wachezaji kwenye hatari
kiafya.
Platini ameiambia BBC kuwa “haiwezi kuwa
mwezi Aprili, Mei wala Juni, bali itakuwa
wakati wa majira ya baridi tu,” na kuongeza
kuwa mwaka 2022 michezo ya nusu fainali na
fainali ya Ligi ya mabingwa Ulaya inaweza
kusogezwa hadi mwezi Juni ikiwa ni lazima,
na kwamba vilabu vinapaswa kukubali uamuzi
wowote utakaokuwa umekubaliwa.
“Sio vilabu ambavyo vinacheza, ni wachezaji
na sio rahisi kucheza mwezi Mei ambapo
kuna joto la hadi 40c” Alisema Platini
mwenye umri wa miaka 59.
Mivutano
Itakumbukwa kuwa Qatar ndiyo ilishinda haki
ya kuwa mwenyeji wa fainali hizo za mwaka
2022 na tangu imeshinda kumekuwa na
mivutano miongoni mwa wadau mbalimbali
kuhusu uwezekano wa kuchezwa nchini humo
kutokana na hali ya hewa ya joto kali.
Sepp Blatter
Rais wa Fifa Sepp Baltter amekuwa
akituhumiwa na baadhi ya watu kuwa
ameipendelea Qatar katika mchakato huo.
Vilabu vikubwa vya ligi kuu ya England, La
Liga ya Hispania na Bundesliga ya Ujerumani
vinadhani kuwa mwezi Mei kutakuwa na nafuu
kiasi wakati ambapo Fifa yenyewe inashikilia
msimamo wa kutafuta uwezekano wa miezi ya
Juni na Julai kama kawaida.
Wadau mbalimbali wenye ushawishi mkubwa
katika soka duniani walikutana jumatatu mjini
Zurich katika harakati za kujaribu kupata
suluhu ya mgogoro huu mkubwa wa aina yake
ulioiweka Fifa njia panda, na wamepanga
kukutana tena mwezi Januari 2015.
Kikosi kazi kimeundwa ili kutafiti na kutoa
mapendekezo yake kwa kamati ya utendaji ya
Fifa mwezi Machi mwaka ujao, huku
pendekezo la Fifa likiwa ni kusogeza fainali
hizo hadi mwezi Novemba na Desemba 2022.
0 comments:
Post a Comment