Ukiwa ni msimu wake wa kumi tu tangu aanze kuichezea klabu ya Barcelona hatimaye mshambuliaji/winga Lionel Messi jana jumamosi usiku alifanikiwa kuifikia na kuivunja rekodi ya ufungaji magoli wa muda wote iliyokuwa ikishikiliwa na Telmo Zarra baada ya kufunga magoli matatu (Hat trick) na kuiwezesha klabu yake kuinyuka Sevilla kwa magoli 5-1.
Messi 27 ambaye hivi karibuni aliweka rekodi nyingine baada ya kufikisha magoli 71 katika michuano ya Ulaya na kumfikia mfungaji wa muda wate wa michuano hiyo nyota wa zamani wa klabu ya Real Madrid Raul Gonzalez Blanco jana alianza kuivunja mapema rekodi ya Zarra baada ya mpira wake wa adhabu kwenda moja kwa moja wavuni dakika ya 21' kisha kuongeza jingine dakika ya 72 na kuhitimisha dakika ya 78 katika mchezo huo mkali uliopigwa katika dimba la Camp Nou mjini Barcelona.
Rekodi hiyo mpya ya Messi ya magoli 253 katika michezo 289 ya La Liga inaivuka ile ya Telmo Zarra nyota wa zamani wa klabu ya Atletico Bilbao aliyoiweka mwaka 1940-55 ya magoli 251 katika michezo 271.Rekodi hiyo imedumu kwa miaka 59 huku nyota kama Diego Maradona,Alfred di Stefano na Johan Cruyff wakishindwa kuifikia na kuivunja licha ya umahiri wao katika kufumamia nyavu za wapinzani.
Messi ameweka rekodi hiyo ikiwa ni miaka kumi tu tangu aanze kuichezea miamba hiyo ya Catalunya hapo mwaka 2004 huku goli lake la kwanza likija Mei 1,2005,baada ya mchezo huo ulioshudia nyota huyo akifunga hat trick yake ya 22 na kufikisha jumla ya magoli 365 katika michuano yote magoli ya Barcelona yalifungwa na Neymar pamoja na kiungo Ivan Rakitic.
Baada ya mchezo huo kuisha Messi aliandika kwenye ukurasa wake wa facebook ambapo pia aliweka video ya goli lake la kwanza la la liga alisema
``Wakati nafunga goli hili sikuwahi kudhani kuwa siku moja ningekuja kuvunja rekodi yoyote ile achilia mbali hii ya Telmo Zarra.Mafanikio haya yamekuja baada ya msaada toka kwa watu wengi sana ambao natumia nafasi hii kuwashukuru na kusema tukio hili ni zawadi kwao"
0 comments:
Post a Comment