JOTO la upinzani kati ya staa wa Real
Madrid, Cristiano Ronaldo na nyota wa
Barcelona, Lionel Messi sasa linaingia
katika uhasama baada ya kudaiwa kuwa
Ronaldo amekuwa akimtukana Messi
pindi akiwa na wachezaji wenzake wa
Real Madrid.
Mwandishi mahiri wa michezo wa
Hispania, Guillem Balague ameandika
katika kitabu chake kuwa Ronaldo
amekuwa akimtukana Messi kwa majina
tofauti na habari hiyo imezua zogo kubwa
nchini Hispania.
Hata hivyo, Ronaldo amesisitiza kupitia
mtandao wake kwamba habari hizo siyo
za kweli na hajawahi kumtukana Messi,
huku akitishia kuchukua hatua za
kisheria.
“Habari zinazunguka zikinishutumu
kwamba nimekuwa nikitoa maneno
machafu dhidi ya Lionel Messi. Habari
hizi ni za uongo na nimemwambia
mwanasheria wangu achukue hatua kwa
wote wanaohusika,” aliandika Ronaldo
katika mtandao wake.
“Nina heshima kubwa kwa wanasoka
wenzangu wote wa kulipwa na Messi
hana tofauti na nao,” aliongeza Ronaldo
mwenye umri wa miaka 29 kwa sasa.
Katika kitabu cha Balague, ameelezea
uhusiano baina ya wachezaji hao wawili
akidai kwamba hawana urafiki wowote
lakini wamekuwa wapole mbele ya jamii
kwa ajili ya kuvifurahisha vyombo vya
habari.
Mwandishi huyo mkongwe amedai
kwamba wachezaji kadhaa wa Real
Madrid wamempa taarifa kwamba siyo tu
Ronaldo amekuwa akimtukana Messi peke
yake, bali mtu yeyote anayemuona
anaongea na Messi.
“‘Ronaldo, labda kwa kuonyesha dalili za
kutopevuka kama ilivyo kwa wanasoka
wengi wa sasa, anadhani kuna umuhimu
wa kuweka sura ya kishujaa mbele ya
wachezaji wenzake na kutomhofia Messi
kwa ajili ya kupambana naye,” anaandika
Balague.
“Lakini yote hayo ni uongo na ndio
maana, kwa mujibu wa baadhi ya
wachezaji wa Real Madrid, Ronaldo
amekuwa akimtukana Messi kwa matusi
mbalimbali na akimuona mtu yeyote
klabuni kwao anaongea na Messi huwa
anaishia kumtukana.”
Kwa sasa Ronaldo yupo katika kikosi cha
Ureno akijiandaa na mechi za kufuzu kwa
Euro 2016 ambapo kesho wanakipiga
dhidi ya Armenia.
Messi jana alikuwa anatarajiwa kuiongoza
Argentina dhidi ya Croatia katika Uwanja
wa West Ham, Rush Green.
Wawili hao wanatazamiwa kukumbana
uso kwa uso Jumanne ya wiki ijayo katika
pambano la kirafiki baina ya nchi zao
litakalopigwa katika Dimba la Old
Trafford.
0 comments:
Post a Comment