728x90 AdSpace

  • Latest News

    Tuesday, April 26, 2016

    HII NDIYO KAULI YA KOCHA WA AZAM FC BAADA YA KUTINGA FAINALI YA KOMBE LA FA

    Dar es salaam,Tanzania.

    KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC,Stewart Hall, amesema kuwa yupo tayari kucheza mchezo wa fainali wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya timu yoyote atayopangiwa nayo ikiwemo kutwaa taji la michuano hiyo.

    Azam FC juzi ilifanya makubwa kwa kutinga fainali ya kwanza ya michuano hiyo tokea iliporejeshwa tena msimu
    huu baada ya kukosekana kwa miaka 14, ikiichapa Mwadui ya Shinyanga kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia dakika 120 kuisha kwa sare ya mabao 2-2.

    Mabingwa hao wanaodhaminiwa na Benki ya NMB, wanasubiria kujua ni timu gani watakayocheza nayo kwenye fainali hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Mei 25 mwaka huu, hii ni baada ya mchezo wa nusu fainali nyingine kuvunjika kufuatia vurugu kubwa iliyotokea ndani ya Uwanja wa Mkwakwani Tanga, wakati huo Yanga alikuwa mbele kwa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union.

    Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Hall alisema
    kuwa bado wanasafari ndefu kuelekea mchezo huo wa fainali na kudai kuwa
    kwa sasa mawazo yake yote yapo katika mechi sita za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) zilizobakia kwa kuhakikisha anashinda zote.

    “Tulikuwa na matatizo mengi tulivyocheza na Mwadui, kwanza kuna
    wachezaji walikuwa na homa, wengine majeruhi na uchovu wa safari ndefu
    kutoka Tunisia na hatukupata muda
    mzuri wa kupumzika, hiyo iliathiri kiwango chetu jana (juzi) na hata mimi sikufikiria kama tunaweza kuonyesha kiwango bora katika mchezo huo hasa kutokana na matatizo hayo, Mwadui wenzetu walikuwa na muda mrefu wa kujiandaa na nilitarajia wangeonyesha kiwango hicho.

    “Malengo tuliyojiwekea katika mchezo huo ni kila mmoja kutimiza majukumu
    yake vema ipasavyo katika eneo lake jambo ambalo tulifanikiwa, lakini kama sio umiliki mpira kupungua katika eneo la kiungo kuelekea mwishoni mwa mchezo huo tungeimaliza mechi mapema kwa kupata ushindi wa bao 1-0 na tusingefika muda wa dakika za nyongeza, hata baada ya dakika hizo mechi ilitakiwa kuisha kwa ushindi wa 2-1 kama sio ubovu wa waamuzi,”alisema.

    Ashangazwa na mwamuzi!!
    Hall aliendelea kushangazwa na maamuzi ya waamuzi wengi wanaochezesha mechi zao msimu huu,hasa baada ya juzi mwamuzi Andrew Shamba kutoka mkoani Pwani kuipa penalti ya utata Mwadui kwenye dakika za mwisho za nyongeza iliyopelekea mchezo huo kuamuriwa
    kwa hatua ya kupigiana mikwaju ya penalti.

    “Waamuzi wengi kuvurunda kwenye mechi zetu imekuwa ikiwapa presha
    sana wachezaji wangu na kutoka nje ya mchezo, sisi kufika hatua ya penalti
    ilikuwa ni utani, sio tu utani bali mwamuzi alisababisha hilo na hii ni baada ya kutoa penalti isiyo halali tena wakati muda wa dakika tano za nyongeza zilizoongezwa ukiwa
    umezidi…Kwa mara nyingine tunaongelea waamuzi, waamuzi na
    tunashindwa kuongelea mpira, hii sio kitu kizuri kwenye soka la Tanzania,”
    alisema..

    Aliongeza kuwa “Nimefurahishwa sana na matokeo tuliyopata,wachezaji wangu wamepigana kwa nguvu na kufanya kazi kwa bidii kwenye mchezo huo, lakini kutokana na waamuzi tumemaliza mechi tukiwa na kadi nyekundu, unajua tumepata kadi za njano na nyekundu kutokana na waamuzi kuwachanganya wachezaji wetu jambo ambalo linachukiza,tumepata matokeo tuliyoyataka lakini tunamkosa David (Mwantika) katika fainali kwa sababu amefungiwa.”

    Tuna nafasi mbili CAF “Kwa sasa baada ya kuingia fainali tumejihakikishia nafasi mbili za kushiriki michuano ya Kimataifa mwakani, tunachoangalia hivi sasa ni
    kushinda mechi zetu sita za ligi zilizobakia hiyo itatupa nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi huku pia tukitakiwa tushinde mchezo huo wa fainali,” alisema Hall.

    Mfumo unambeba Mcha
    Kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ na
    Sofapaka ya Kenya, amefurahishwa na kiwango kizuri kinachoendelea kuonyeshwa na mshambuliaji wake Khamis Mcha ‘Vialli’, aliyefunga
    mabao mawili pekee ya Azam FC katika mchezo huo.

    “Amefunga mabao matatu sasa katika mechi nne zilizopita, kwa sasa
    hatuutumii mfumo wa 3-5-2 ambao umekuwa hauendani naye, kutokana
    na kutokuwa na uwezo wa kucheza nafasi ya beki wa pembeni mwenye kazi nyingine ya kuwa kama winga (wingbacks), kwa sababu sio mtu wa ulinzi, hivi sasa tunatumia mifumo
    miwili 4-3-3 na 3-5-2 tukiwa tunaibadilisha mara kwa mara, Mcha anaendana sana na mfumo wa 4-3-3 na kila tunapoutumia amekuwa
    akifunga mabao.

    “Tumefurahishwa naye sana kwa sababu ni mchezaji mzuri sana
    kuanzia mazoezini, pia ni kijana profesheno na hata asipokuwepo kikosini amekuwa akifanya kazi kwa nguvu na bidii zaidi, kiukweli amenifurahisha sana,” alisema.



    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: HII NDIYO KAULI YA KOCHA WA AZAM FC BAADA YA KUTINGA FAINALI YA KOMBE LA FA Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top