SEHEMU YA KWANZA: NI MANCHESTER
DERBY NI MOURINHO VS GUARDIOLA.
Na.Chikoti Cico.
Saa 8:30 mchana kwa sasa za Afrika
Mashariki hapo siku ya Jumamosi macho na masikio ya wapenzi wa soka duniani
yataelekezwa jijini Manchester kufuatilia mtanange wa shoka kati ya Manchester
United vs Manchester City.
Ni mchezo ambao unawakutanisha
marafiki wa zamani lakini maadui wa sasa, ni Jose Mourinho vs Pep Guardiola,
makocha wawili wenye falsafa mbili tofauti lakini wenye nia moja ambayo ni
ushindi peke yake. Vikosi vya makocha hawa vimegharimu zaidi ya pauni milioni
670 hivyo ukiachana na mchezo wenyewe ni dhahiri huu ni mchezo unaovikutanisha
vilabu vyenye kujua kutumia pesa kwenye gulio la usajili wa nyota mbalimbali.
Huu utakuwa mchezo wa 17
kuwakutanisha Mourinho na Guardiola ambapo katika michezo 16 waliyokutana kabla
katika vilabu vitano tofauti Mourinho ameshinda mara tatu, Guardiola akishinda
mara saba na wametoka sare mara sita hivyo kitakwimu Guardiola mpaka sasa ni
kiboko ya Mourinho.
Ukiachana na takwimu hizo makocha
hawa wanabaki kuwa makocha wawili mahiri kabisa ktk ulimwengu wa soka huku kila
mmoja akiwa amejikusanyia tuzo na vikombe mbalimbali katika mashindano kadha wa
kadha. Pia ukiachana na kwamba hii itakuwa “Manchester Derby” ya 172, huu
utakuwa mchezo wa kuionyesha dunia kwa mara nyingine kati ya makocha hawa
wawili nani ana “taktiki” bora zaidi kuweza kuipa timu yake ushindi, hii ikiwa
ni sifa kubwa kila mara Mourinho na Guardiola wanapokutana.
Baada ya michezo mitatu ya ligi ya
primia ambayo United na City wameshinda na kujikusanyia alama 9, huu utakuwa ni
kama mchezo mwingine wa kufungua pazia la ligi hiyo ni kama kusema sasa ligi
ndiyo inaanza ndani ya jiji la Manchester kutokana na uzito wa mchezo wenyewe
na makocha husika.
Mpaka sasa Mourinho anayo picha
iliyopigwa mwaka 1997 baada ya mchezo wa fainali ya “European Cup Winners Cup”
kati ya Barcelona vs PSG wakati huo Mourinho akiwa sehemu ya benchi la ufundi
la Barcelona chini ya Bobby Robson na Guardiola akiwa kiungo wa klabu hiyo.
Picha hiyo inawaonyesha Mourinho na Guardiola
wakiwa wamekumbatiana kwa furaha, ni ngumu kufikiria kama makocha hawa wawili
ambao kwa sasa ni kama chuma na kutu wanaweza kuwa waliwahi kukumbatiana,
urafiki wako uliokuwepo kabla kitambo ulifikia tamati toka Guardiola alipopewa
kuifundisha Barcelona nafasi ambayo Mourinho ndiye aliyekuwa akipigiwa chapuo.
Kuelekea “Manchester Derby” maneno
ya Zlatan Ibrahimovic moja ya wachezaji ambae anawafahamu vyema makocha hawa
wawili yanaweza kutoa picha ya namna makocha hawa walivyo, kwa maneno yake
mwenyewe akiwa anawaelezea makocha hawa Zlatan amewahi kusema “Kama Mourinho analeta mwanga ndani basi
Guardiola yeye hushusha mapazia kuleta giza”
.
SEHEMU YA PILI. NI MANCHESTER DERBY,
NI MOURINHO VS GUARDIOLA.
Timu zote mbili za jiji la Manchester
zimeshaweka kibindoni alama tisa toka pazia la ligi ya Uingereza kufunguliwa,
huku United wakifunga magoli sita na kufungwa goli moja nao City wakifunga
magoli tisa na kufungwa magoli matatu.
Kwa namba hizo “hafifu” za magoli ya
kufunga na kufungwa kwenye michezo mitatu ya ligi ya primia unaweza kusema
mpaka sasa United wana UKUTA mzuri zaidi kuliko City, wakati wao City
wakionekana kuwa na safu nzuri ya USHAMBULIAJI kuliko United. Kuelekea mchezo
huo kuna maeneo mbalimbali ambayo yanaweza kuamua mbabe wa “dabi” hii kuanzia
eneo la ulinzi mpaka eneo la ushambuliaji ukiachana na sababu zingine za nje ya
uwanja kama vile United kuwa wenyeji.
WACHEZAJI WA KUCHUNGWA ZAIDI.
Zlatan Ibrahimovic- Akiwa na hamu ya kutaka
kumwonyesha Guardiola kwamba alikosea kumpeleka kwa mkopo na kumuuza mwaka 2010
wakati akiwa Barcelona. Ibra ni mchezaji wa kuchungwa sana hasa ukizingatia
kwamba mpaka sasa katika michezo mitatu ya ligi tayari ameshafunga magoli matatu.
Akiwa na umri wa miaka 34 bado
ameonyesha anayo njaa ya mafanikio chini ya kocha ambaye ni kipenzi chake Jose
Mourinho na hivyo City wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kumzuia mshambuliaji
huyu, ni moja ya wachezaji ambao wanaweza kuamua matokeo ya Manchester dabi.
Wayne Rooney- Pamoja na kwamba nahodha huyu wa United anaonekana kupwaya tokea
kuanza kwa ligi ya primia msimu huu lakini bado huwezi kumchukulia kawaida
Rooney ukizingatia kwamba amezitikisa nyavu za City mara 11 katika michezo
mbalimbali aliyocheza dhidi yao.
Na pia katika mechi kama hizi ambazo
unaweza kuziita “mechi kubwa” wachezaji aina ya Rooney yaani wachezaji
“wakubwa” na wenye uzoefu huwa ndiyo huamka kuleta utofauti na hata kuamua
matokeo hivyo Rooney pia anatakiwa kuangalia kwa jicho la tahadhari. Raheem
Sterling- Kama kuna mchezaji ambaye ndani ya mwezi mmoja amefanya Guardiola
apewe mshahara wake bila maswali basi ni huyu, Sterling ambaye alikuwa anafifia
wakati msimu uliopita unafikia tamati amefufuka tena chini ya kocha huyu mpya,
beki za United zinatakiwa kukaa sawasawa kumzuia huyu winga machachari.
David Silva- Kiungo huyu mpole
mwenye mguu wa kushoto wa dhahabu ndiye hasa injini ya Guardiola katika kuamua
mpira uende wapi na kwa wakati gani, chini ya kocha mpya Silva amekuwa akikava
eneo kubwa la uwanja huku akiwa na jukumu la kuchukua mpira kutoka kila pembe
ya uwanja na kuanzisha mashambulizi huku akitafuta mashimo ya kupiga pasi za
mwisho.
Viungo wa Manchester United kwenye
eneo la katikati hasa Fellaini watakuwa na kazi kubwa kumzuia mchezaji huyu,
kama wakimpa nafasi ya kutawala eneo hilo basi Manchester dabi itaamuliwa na
Silva. Huku Bailly kule Stones, wote wana umri wa miaka 22 lakini mpaka sasa ni
mabeki ambao makocha wa timu zote mbili wanawategemea katika kuzifanya ngome
zao kuwa salama lakini zaidi sana kuleta utulivu kwenye timu zao kutokea eneo
la nyuma.
Bailly pia atakuwa na kazi kubwa ya
kupambana na yeyote kati ya Nolito ama Sterling ambao mmoja kati yao anaweza
kucheza kama mshambuliaji wa katikati baada ya Aguero kusimamishwa na huku
Stones akiwa na jukumu zito dhidi ya Ibrahimovic jukumu ambalo linaweza kuamua
nani ataibuka mbabe kati ya timu hizi mbili.
Kwa ujumla Manchester Dabi ya msimu
huu inaweza kuwa ndiyo dabi itakayokuwa na msisimko zaidi mbele ya mashabiki wa
klabu zote mbili na wapenzi wa soka duniani kote na kama itaweza kufikia kilele
cha juu kabisa cha ubora na ushindani inawezekana kwa miaka ambayo Mourinho na
Guardiola watakuwa ndani ya ligi ya primia basi Uingereza wakawa wamejipatia
“EL CLASICO” yao.
0 comments:
Post a Comment