Dar Es Salaam,Tanzania.
Baada ya klabu ya Yanga kutoka Sare na Ndanda FC ugenini , uongozi wa Yanga umeanza kutoa malalamiko na kudai Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halijawatendea haki kwenye upangaji wa ratiba.
Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, alisema kuwa kasoro hizo za ratiba walianza kuziona mapema na kupeleka kilio chao TFF lakini hakuna marekebisho yoyote yaliyofanyika.Deusdedit alisema kuwa haiwezekani Yanga ambao juzi ilicheza Mtwara mechi yake inayofuata itacheza Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru wakati mahasimu wao Simba ambayo hawajasafiri wenyewe watateremka uwanjani Jumapili kuikaribisha Mtibwa Sugar.
“Ratiba ya msimu huu haina uwiano mzuri kabisa, haiwezekani timu ambayo ilikuwa mkoani ikatakiwa kuanza kucheza Jumamosi na Simba ambao jana (juzi) wamecheza hapa hapa Dar es Salaam watacheza Jumapili, hapo inahitaji kutumia mtaalamu kutoka nje ya nchi ili aje kutusaidia kupanga ratiba au kufanya
marekebisho?,” alihoji katibu huyo.Alilalamika pia timu yao haijatendewa haki katika mechi zao mbili zitakazofanyika Shinyanga kupishana siku saba na kutakiwa kubakiwa na siku nne kwa ajili ya kurejea Dar es Salaam kujiandaa dhidi ya Simba.
“Tuliomba tufanyiwe marekebisho lakini hakuna kilichofanyika mpaka sasa, hiyo ndiyo shida ambayo inatukabili msimu huu,” alisema kiongozi huyo.Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu, Hamad Yahaya, alisema kuwa duniani kote hakuna timu ambayo itaridhika na ratiba na hali hiyo iko katika kila klabu.
Wakati huo huo, kocha mkuu wa Yanga,Hans van der Pluijm, amesema kuwa hali ya uchovu uliwaathiri wachezaji wake katika mechi yao dhidi ya Ndanda ilimalizika kwa sare ya 0-0.Pluijm alisema pia wenyeji walijiandaa kucheza soka la ‘kutibua’ kila walipoona wachezaji wa Yanga walipokuwa na mpira na hivyo kuharibu mashambulizi yao.Mabingwa hao watetezi ambao wana kiporo cha mechi moja dhidi ya JKT Ruvu sasa wamefikisha pointi nne baada ya kuteremka uwanjani mara mbili.
0 comments:
Post a Comment