Kampala,Uganda.
UNAWEZA usiamini lakini hii ndiyo hali halisi ya jinsi na namna soka la Afrika Mashariki linavyoendeshwa.
Kocha raia wa Serbia ,Micho Sredojevic,ambaye Jumapili iliyopita aliiwezesha Uganda kufuzu fainali za AFCON baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka 38 hajalipwa mishahara yake kwa kipindi cha miezi mitano sasa.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda ni kwamba Micho analidai shirikisho la soka la nchi hiyo (FUFA) zaidi ya dola za Marekani elfu 60,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni 235 za Uganda.
Kiasi hicho ni kutoka katika malimbikizo ya mshahara wake wa dola elfu 12,000 (Shs40m) anaolipwa kwa mwezi pamoja na bonasi mbalimbali.
Daily Monitor limeendelea kutanabaisha kuwa licha ya Micho majuzi kulipwa bonasi zake kufuatia kuiwezesha Uganda kufuzu michuano ya AFCON bado kocha huyo anadai bonasi zake mbili za michezo iliyopita ya kuwania tiketi ya CHAN dhidi ya Sudan pamoja na ile ya kombe la dunia dhidi ya Togo ambayo inakadiriwa kufikia dola elfu 8,000 (Shs27m)
Aidha Daily Monitor limeongeza kuwa FUFA pia imeshindwa kumgharamia kocha huyo tiketi za ndege za kwenda likizo kwao Serbia na kurudi Uganda kwa kipindi cha miaka miwili sasa.
Mkataba wa Micho na FUFA unaagiza kuwa kocha huyo wa zamani wa vilabu vya St.George na Yanga SC anapaswa kulipiwa usafiri wa ndege kwenda likizo kwao Serbia angalau mara moja kwa mwaka.
0 comments:
Post a Comment