Mbeya.Tanzania.
PATACHIMBIKA!
Ndivyo hali itakavyokuwa ndani ya Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, leo Jumamosi pale Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC,
itakapokuwa ikisaka pointi tatu muhimu dhidi ya wenyeji wao Mbeya City.
Mchezo utakaoanza saa 10.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Azam FC itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi dhidi ya
Tanzania Prisons (1-0) huku Mbeya City nayo ikitoka kuichapa Mbao ya
Mwanza 4-1 katika Uwanja wa CCM, Kirumba Mwanza.
Ubora wa pambano hilo unaongezwa na vita nyingine ya kukaa kileleni,
kwani timu zote hizo zina pointi sawa saba kileleni zikifafanana kwa
kila kitu, lakini Azam FC ipo juu kutokana na jina lake kutangalia
kiherufi. Simba nayo ina pointi kama hizo lakini imezidiwa tofauti ya
mabao ya kufunga na kufungwa (GD).
Ushindi wowote wa Azam FC kesho utaihakikishia nafasi ya kukaa
kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya pointi tatu dhidi ya Mbeya City,
huku ikiwasubiria wapinzani wake wa karibu Simba, watakaocheza na Mtibwa
Sugar Jumapili ijayo (Septemba 11).
Zeben asema ni pointi tatu tu
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz
Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, alisema kikosi chake kipo
vizuri na anaimani kubwa wataibuka na ushindi mwingine dhidi ya timu
hiyo kabla ya kurejea Dar es Salaam.
“Timu iko vizuri na mazoezi yanaendelea vizuri, tumejaribu kufanya
tathimini ya mchezo uliopita (Tanzania Prisons) na kufanyia marekebisho
kadhaa na tunaamini kuwa tutapata pointi nyingine tatu kesho,” alisema.
Azam FC itaendelea kuwakosa nyota wake watatu, mabeki Pascal Wawa,
Aggrey Morris na mshambuliaji Francisco Zekumbawira, ambao bado
wanaendelea na programu za mazoezi mepesi kabla ya kurejea dimbani.
Afurahishwa kuvunja rekodi
Katika hatua nyingine, Zeben alifurahishwa na baadhi ya rekodi
walizofanikiwa kuvunja msimu huu ile ya kutwaa taji la Ngao ya Jamii
dhidi ya Yanga na juzi kuifunga kwa mara ya kwanza Tanzania Prisons
(1-0) ndani ya Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Azam FC hadi inatwaa kwa mara ya kwanza taji hilo ilikuwa haijawahi
kuifunga Yanga kwenye fainali tatu mfululizo, lakini Zeben ameweza
kukiongoza kikosi hicho kulitwaa, vilevile juzi imeifunga kwa mara ya
kwanza Prisons jijini Mbeya tokea ipande daraja Julai 27, 2008.
“Benchi zima limefurahishwa kwa kuifunga Yanga na juzi Tanzania
Prisons, tunafurahia pia kuisaidia klabu kufikia malengo hayo kwa mara
ya kwanza, lakini kwa sasa kilichombele yetu ni mechi ya kesho, Yanga
tumeshaachana nayo na pia ya Prisons yameshapita, tunachoangalia ni
mchezo wa kesho namna gani tunaweza kuchukua pointi tatu muhimu,”
alisema.
Rekodi zao (Head to Head)
Mara ya mwisho kukutana timu hizo msimu uliopita, Azam FC ilipata
ushindi kwenye mechi zote mbili, ikianza kwa kuichapa mabao 2-1 katika
Uwanja wa Azam Complex kabla ya kuishushia kipigo kikali cha 3-0 ndani
ya Uwanja wa Sokoine Februari 20 mwaka huu.
Kitakwimu mpaka sasa kwa mujibu wa rekodi tokea timu hizo zianze
kukutana baada ya Mbeya City kupanda daraja mwaka 2013, Azam FC ndio
imeonekana kuwa mbabe ikishinda mechi nne kati ya sita walizocheza hadi
sasa huku mechi mbili zikienda sare.
Jumla ya mabao 18 yamefungwa ndani ya mechi hizo sita, Azam FC
ikifunga robo tatu ya mabao hayo (12) na Mbeya City ikitupia matano tu.
Mechi za kukumbukwa
Mechi pekee zitakazoendelea kukumbukwa tokea timu hizo zianze
kukutana ni ile ya Aprili 13, 2014, ambayo Azam FC ilishinda mabao 2-1
na kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
(VPL) ndani ya Uwanja wa Sokoine, ikilibeba kwa mara ya kwanza
kihistoria bila kufungwa mchezo hata mmoja.
Pambano lingine ni lile la Novemba 7, 2013, lililofanyika ndani ya
dimba la Azam Complex na kuisha kwa sare ya mabao 3-3, huku ikishuhudiwa
hat-trick pekee ya mshambuliaji wa Mbeya City, Mwagane Yeya, ambayo
bado inasimama mpaka sasa katika mechi walizokutana.
0 comments:
Post a Comment